Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 2 JELA KWA KUMUUA BABA YAKE BILA KUKUSUDIA
07 Mar, 2025
AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 2 JELA KWA KUMUUA BABA YAKE BILA KUKUSUDIA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Sumbawanga imemuhukumu Kiumbe John Kantanga (28)  kifungo cha miaka 2 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumuua baba yake mzazi bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 5 Machi 2025 na Hakimu Mwandamizi na mwenye Mamlaka ya Ziada Luambano baada ya kuridhika na kiri ya mshtakiwa na maelezo ya shauri.

Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 16279 ya mwaka 2024,Bw. Kiumbe ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bumanda, wilaya ya Nkasi mkoa wa Rukwa alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuua bila ya kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe  25 Mei, 2024 katika kijiji cha Bumanda, wilaya ya Nkasi ambapo inadaiwa mshtakiwa alimpiga shoka baba yake baada ya kutamkiwa maneno yaliyomfanya kujawa na jazba.

Kesi hii imeendeshwa na japo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Ladislaus Akaro akisaidiana na Mwanaisha Liwawa.