AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 20 JELA KWA SHAMBULIO LA AIBU DHIDI YA BINTI MWENYE UMRI WA MIAKA 13

Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es salaam imemhukumu Hilary Benard Matia (37) kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la shambulio la aibu dhidi ya binti mwenye umri wa miaka kumi na tatu (13).
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na Hakimu wa Mahakama hiyo Mhe. Vicky Mwaikambo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 2969/2024 ya Bw. Benard ambaye ni mkazi wa Toangoma Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la Shambulio la aibu (grave sexual abuse) kinyume na kifungu cha 138C(1) (a) and (2) (b) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)
Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 01 December, 2023 katika eneo la Kongowe Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam ambapo inaidaiwa siku ya tukio mshtakiwa kwa tamaa za kimwili alimnyonya mdomo mhanga ambaye ni mwanafunzi wake.
Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Sabina Ndunguru akisaidiana na Nicas Kihemba.