AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA KUZINI NA MAHARIM

Mahakama ya Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam imemhukumu Bw. Silvester Michael Chihongwe (42) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka miwili
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na Mhe. Catherine Madili baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 9568/2024, Bw. Silvester ambaye ni mkazi wa Kurasini, Shimo la Udongo Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuzini na Maharimu (incest) kinyume na kifungu cha 158(1) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)
Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 22 Machi, 2024 katika eneo la Kurasin, Shimo la Udongo Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam ambapo inadaiwa mama wa mtoto huyo alikwenda kuchota maji aliporudi alikuta tayari mtoto huyo amefanyiwa kitendo hicho na baba yake mzazi.
Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Abdon Andrew Bundala akisaidiana na Shabani Twahil Shaban.