AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA, KULIPA FIDIA YA MILIONI MOJA NA VIBOKO SITA KWA KWA UBAKAJI

Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam imemhukumu Bw. Arafath Laurence Thadei kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya kiasi cha shilingi milioni moja pamoja na kuchapwa viboko sita wakati wa kuingia gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka Manusura mwenye umri wa miaka 15.
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 27 Februari, 2025 na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam Mhe. Janeth Mtega baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 22093/2024 Bw. Thadei ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la ubakaji kwa Manusura kinyume na kifungu cha 130(1),(2) (a) na 131 cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)
Mtuhumiwa alitenda kosa hilo katika tarehe zisizojulikana kati ya mwezi wa 12 mwaka 2023 na tarehe 4 Machi 2024 katika eneo la Tungi,Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam ambapo inaidaiwa alimuingilia kimwili binti wa miaka kumi na tano(15).
Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Bw. Sayi Gugah akisaidiana na Epiphania Mushi.