ALIYEMUUA MKEWE KISHA KUMCHOMA KWA MAGUNIA YA MKAA AHUKUMIWA KUNYONGWA

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam imemhukumu mfanyabiashara Bw. Hamis Said Luwongo mwenye umri wa miaka 38 kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa aliyejulikana kwa jina la Bi. Naomi Marijani kisha kuchoma mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 26 Februari, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi 14 na vielelezo 10 kutoka upande wa Mashtaka.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la Mawakili wa Serikali wawili likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Yasinta Peter akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Bi. Ashura Mnzava, waliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa wale wanaofanya ukatili dhidi ya wanawake wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye ndoa.
"Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili na kinaleta mashaka kwa wanawake waliopo katika ndoa na wanawake wanaoingia katika ndoa, hivyo tunaomba Mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wanaume wanaotumia kigezo cha ndoa kufanya ukatili kwa wake zao.” Amesema Wakili Mnzava.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 44/2023, Bw. Hamis Luwongo ambaye ni mkazi wa Gezaulole, Wilayani Kigamboni, Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ya mkewe Naomi kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 15 Mei, 2019 nyumbani kwao, kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku ambapo inadaiwa masalia ya mwili na majivu aliyachukua akaenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake kwa lengo la kuficha ushahidi.