DCI AHIMIZA KUUNGANISHA NGUVU NA WADAU WENGINE

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bw. Ramadhani Kingai amesema ni muhimu kikao cha Taasisi zinazounda Utatu kuwafikiria na kuwaunganisha wadau wengine kwa kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanafanya jambo ambalo linawasaidia wananchi na kurahisisha maisha yao hususani kwenye masuala ya ufuatiliaji wa haki za msingi kwa mujibu wa sheria zilizopo.
"Kuwa pamoja kunasaidia kurahisisha mawasiliano na kuwezesha mambo mengine kuendelea sawasawa."
DCI Kingai amebainisha hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu ( Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kilichofanyika tarehe 8 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Ramadhani amesema kikao hicho kitajadili masuala mbalimbali yanayohusu utoaji wa haki nchini ambayo yaliibuliwa wakati wa ukaguzi wa pamoja uliofanyika mwaka huu 2024 kwa lengo la kuhakikisha wanaboresha utendaji kazi wao lakini pia utoaji wa haki kwa ajili ya Watanzania.
"Tutapitia utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita ambayo yatatupa mwanya wa kujitathmini utendaji wetu wa kazi kwa mwaka mzima. Baada ya kupitia maazimio hayo wajumbe wote wa kikao tutakuwa na fursa ya kuona nini kilifanyika na nini hakikufanyika ili kuweka mpango kazi kuhakikisha tunaleta mafanikio chanya." Amefafanua hayo DCI Kingai
Aidha Mkurugenzi huyo ameitaka Menejimenti kuwa na umoja katika kazi ili kujenga vyema jukwaa la haki jinai ambapo Taasisi hizo tatu ni muhimili katika kutekeleza jukumu la kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Ni matumaini yangu kuwa kikao hiki cha Menejimenti kitatoka na maazimio mahususi ambayo yataenda kuwasilishwa kwa watendaji wetu na kutumika kama dira katika kuboresha utendaji kwa mwaka mwingine." Ameyasema hayo DCI Kingai.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Crispin Chalamila ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali na kuyasimamia yale yote ambayo watakubaliana kama Utatu kwani umoja huo ni muhimu sana katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao waliyopewa dhamana ya kuyasimamia.