Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

DPP AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA MAHABUSU GEREZA LA KEKO
21 Nov, 2024
DPP AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA MAHABUSU GEREZA  LA KEKO

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameahidi kushughulikia changamoto na kero zinazowakabili mahabusu na wafungwa waliopo katika gereza la keko Jijini Dar es saalam.

DPP Mwakitalu amebainisha hayo tarehe 19 Novemba, 2024 mara  baada ya kukagua na kuzungumza na mahabusu waliopo katika gereza hilo.

Katika hatua nyingine Bw. Sylvester Mwakitalu, amesema kuwa mazungumzo yaliyofanyika na mahabusu katika gereza hilo yamekuwa yenye manufaa makubwa kwani yatasaidia kurekebisha na kuboresha utendaji wa kazi na changamoto zote zilizowasilishwa zitashughulikiwa mapema na kwa masuala yanayohitaji mabadiliko ya sheria nayo yatawasilishwa katika Mamlaka husika ili yaweze kushughulikiwa.

Akizungumza na vyombo vya habari Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Aretas Lyimo, ametoa onyo kwa watuhumiwa watakaoachiwa au kumaliza vifungo vyao kutorudia kutenda makosa bali wasaidiane na serikali katika kuiletea nchi maendeleo na wafanye kazi halali ili kujiongezea kipato.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Cyprian Chalamila amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kupokea changamoto zinazowakabili watuhumiwa waliopo katika mahabusu hiyo na kuchukua hatua za kushughulikia changamoto zilizowasilishwa ili sio tu haki itendeke bali ionekane ikitendeka.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bw. Ramadhani Kingai amesema kuwa atashughulikia changamoto za kiupelelezi ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Naye Mkuu wa gereza la Mahabusu la Keko, Kamishna Msaidizi Juma Mgumba amemshukuru Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu na timu aliyoambatana nayo katika ziara huku akieleza kuwa upelelezi ukikamilishwa mapema na kesi zikasikilizwa na kuisha kwa wakati itasadia watuhumiwa kujua hatma yao  na msongamano katika gereza hilo kupungua au kuisha kabisa.