Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

DPP AWASHUKURU WADAU KWA USHIRIKIANO
14 Feb, 2025
DPP AWASHUKURU WADAU KWA USHIRIKIANO

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewashukuru wadau wanaofanya kazi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwepo Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Katiba na Sheria, Mkurugenzi Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika maandalizi na uzinduzi wa Mwongozo wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashauri ya Makosa ya Kimtandao.

Mkurugenzi wa Mashtaka, ametoa shukrani hizo Tarehe 13 Februari 2025 wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa kushughulikia Kesi za Mtandao kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka, ambapo amesema lengo la mwongozo huo ni kuboresha utendaji kazi kwa kuweka namna iliyo sawa ya kushughulikia kesi za mtandao hivyo kuwawezesha Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kushughulikia kesi za hizo kwa ufanisi na tija. 

Pia amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inaahidi kutekeleza sera, sheria na kanuni mbalimbali zilizopo katika kupambana na uhalifu wa makosa ya kimtandao kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kuwa watu wanaojihusisha na uhalifu wa kimtandao  wanashughulikiwa ipasavyo.

Alisema licha ya kuweka namna sawa ya ushughulikiaji wa kesi za mtandao, Mwongozo huu utarahisisha na kuleta ufanisi katika upelelezi na uendeshaji wa kesi za Mtandao.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imesimama kama kiongozi katika kuandaa Mwongozo huo, ikiwa ni pamoja na kutambua ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi na Wizara anayoiongoza.

"Hili linatupa faraja ya kuona ya kwamba shughuli hii ya kupambana na uhalifu wa kimtandao haipo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pekeyake. Uwepo wako kwa siku ya leo unatupa dhamira ya dhati uliyonayo ya kwamba kwa pamoja tunaunganisha nguvu zetu na kupambana na uhalifu wa kimtandao." Amefafanua Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Akitoa neno la utangulizi juu ya uzinduzi wa Mwongozo huo, Mkurugenzi Divisheni ya Utaifishaji na Urejeshaji Mali Makosa yanayovuka Mipaka na Uhalifu Mahsusi, Bw. Faraja Nchimbi alisema Mwongozo huo unalenga utendaji wa ndani wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Vyombo Chunguzi kwa ajili ya kuwaongoza na kuweka viwango (Standards) kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka katika Upelelezi na Uendeshaji wa mashauri ya Makosa ya Kimtandao na Makosa mengineyo yanayoshabihiana nayo.

Alisema Uandaaji wa mwongozo ulizingatia maeneo yenye changamoto za utendaji wa kila siku ili kuongeza ufanisi wa kazi kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka ili kuondokana na dosari za kiutendaji wakati wa kushughulikia makosa ya jinai katika maeneo ya upelelezi na uendeshaji wa Makosa ya Kimtandao.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi Joshua Mwangasa ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bw. Ramadhani Kingai ametoa pongezi kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kufanikisha kuandaa Mwongozo huo kwani itawasaidia kuwaongoza kutatua changamoto katika kupeleleza na kuchunguza makosa ya kimtandao.

"Ni furaha yetu kama Jeshi la Polisi kuona Mwongozo unakwenda kutekelezeka ili kuweza kusaidia katika kukabiliana na makosa ya kimtandao." Amefafanua Kamishna Msaidizi wa Polisi.”

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Sheria wa TAKUKURU Bw.  George Barasa ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Chalamila amesema TAKUKURU imekuwa ikiathirika katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia shughuli za mitandao juu ya uhalifu unaofanyika mitandaoni, vitendo vingi vya rushwa vinafanyika kupitia mtandao hivyo mwongozo huo utakuwa ni nyenzo muhimu sana ambayo itakwenda kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake katika kupambana na rushwa.