JELA MIAKA 40 KWA KOSA LA WIZI

Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Mbeya imemhukumu Charles Ezekiel Chauga kutumikia kifungo cha miaka 40 gerezani.
Hukumu hiyo imesomwa tarehe 29 Agosti, 2025 na Hakimu Paul Rupia baada ya kuridhika na ushahidi uliwasilishwa na Jamhuri.
Katika kesi hiyo ya Jinai Na. 15712 ya mwaka 2025, Bw. Chauga ambaye ni mkazi wa Wilaya na Mkoa wa Mbeya alikuwa anakabiliwa kwa mashtaka manne ya Wizi wa uwakala Kinyume na Kifungu cha 273(b) cha Sheria ya Kanuni ya adhabu,(Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022).
Mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya mwezi Januari, 2024 mpaka tarehe 4 Novemba, 2024 akiwa wakala na msimamizi katika kampuni ya kifedha inayofahamika kwa jina la Iman Super Dealer Company Limited iliyopo maeno ya Mafiati ndani ya Wilaya na Mkoa wa Mbeya ambapo imethibitika kuwa mshtakiwa akiwa mfanyakazi katika kampuni hiyo alipewa majukumu ya kushughulika na wateja wa nje na ndani ya kampuni, kuweka fedha kwenye akaunti mbalimbali za kibenki kama CRDB, NMB, NBC, M PESA 1 na 2, TIGO, LUKU, A SUPER, VODA SUPER, pamoja na AIRTEL zinazomilikiwa na kampuni hiyo pamoja na kukabidhiwa linę ya Mpesa kwa ajili ya kusambaza Pesa kwa mawakala mbalimbali wa huduma za kifedha.
Mnamo tarehe 4 Novemba 2024 mshtakiwa alifika ofisini ambapo baada ya muda aliondoka ofisini bila kukabidhi hesabu za kifedha za kila siku kama majukumu yake yanavyoeleza, ndipo Meneja wa kampuni hiyo aliwasiliana nae ambapo mtuhumiwa aliahidi kurudi akidai ameelekea benki na angekabidhi hesabu baadae akirudi ofisini lakini muda ulipita na mshtakiwa hakurudi ndipo uongozi ulipata shaka kutokana na kushndwa kumpata kwa muda mrefu na kuamua kupiga hesabu za mtaji mzima wa ofisi na Kubaini kwamba kiasi cha shillingi Milioni hamsini na tatu na elfu kumi (53,010,000/= )Tshs. zimepotea katika mtaji wa kampuni hiyo ambazo zilikuwa chini ya usimamizi wa mtuhumiwa kutokana na nafasi yake kama msimamizi wa ofisi hiyo.
Mshtakiwa baada ya kutenda tukio hilo alikimbilia mkoa wa Morogoro ambapo mawakala watatu walifika ofisini na kudai kiasi cha fedha cha jumla ya shilingi Milioni kumi na mbili (12,000,000/=) Tshs. ambazo walimkabidhi mshtakiwa Mnamo tarehe 2, 3 na 4 ya Mwezi Novemba, 2024 kutokana na nafasi yake ya kazi kwenye kampuni hiyo ili aweke fedha hizo kwenye akaunti za benki ikiwemo NMB, CRDB na NBC lakini mshtakiwa hakufanya hivyo na kufanikiwa kuiba kiasi hicho cha fedha.
Mnamo tarehe 12 Novemba, 2024, mshtakiwa alikamatwa maeneo ya Tuliani Mkoani Morogoro na Kufikishwa kituo cha polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Jumla ya mashahidi nane (8) wa upande wa Jamhuri walitoa ushahidi na mtuhumiwa alijitetea mwenyewe.
Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.