KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA SERIKALI UJENZI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA TEMEKE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Mikoa na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kusogeza huduma kwa wananchi pamoja na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma za mashtaka ya jinai nchini jambo litakalosaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi na kulinda amani na Usalama ambayo ni dhamira ya Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kukagua maendeleo ya Miradi ya ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Mikoa ya Kimashtaka Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Machi, 2025 Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe. Dkt. Joseph Mhagama alieleza kuwa Kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hizo za Mikoa ya Kimashtaka Temeke na Kinondoni ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2025
Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa maono na utashi wa kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati na kueleza imetokana na uongozi bora wa viongozi waliopo.
“Mimi ni Wakili hadi sasa, nimefanya kazi ya Uwakili kwa miaka zaidi ya 30 na nimefanya kazi na Wakurugenzi wa Mashtaka wengi, lakini nikupongeze Mkurugenzi wa Mashtaka Mwakitalu kwa mageuzi haya makubwa ambayo yanahitaji utashi mkubwa, uadilifu na kujitoa."
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alimshukuru Mhe. Rais, Kamati ya Bunge na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya mageuzi haya muhimu na kueleza kwamba miradi inayoendelea kutekeleza ni matunda ya Kamati hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa miradi hii ni sehemu ya Miradi inayoendelea kutekelezwa katika mikoa mingine ambayo ipo katika hatua mbalimbali na kwamba kuanzia mwaka huu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeanza pia kutekeleza miradi ya Ujenzi ya Ofisi za Mashtaka za Wilaya ambapo tayari imeanza katika Wilaya 24 ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa pongezi kwa kutekelezwa kwa miradi katika Wilaya hizo na kuongeza kwamba itakua na tija kwa Wananchi.
" Tuna imani kuwa mradi huu ukikamilika kwa wakati utaweza kusaidia sana Watanzania, ambao wanausubiri kwa hamu kubwa sana." Amefafanua Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Mhagama alisema Kamati inaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo itachochea upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa usimamizi mzuri wa taasisi zake katika utekekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali.
Sambamba na hilo alitoa rai kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa asilimia 100 kwa ufanisi ndani ya muda uliopangwa kulingana na mkataba uliopo.