Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

KOSA LA WIZI WAMPELEKA JELA MIAKA 14
04 Sep, 2025
KOSA LA WIZI WAMPELEKA JELA MIAKA 14

Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Mbeya imemhukumu Geofrey  Victor Nyenza kutumikia kifungo cha miaka 14 gerezani kwa kosa la kuvunja nyumba na kuiba.

Hukumu hiyo imesomwa tarehe 29 Agosti,  2025 na Hakimu  Paul Rupia baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri.

Katika kesi hiyo Na. 16964 ya mwaka 2025, Bw.  Victor Nyenza ambaye ni mkazi wa  Mtaa wa Chem Chem Kata ya Igawilo iliyopo ndani ya  Wilaya na Mkoa wa Mbeya alikuwa anakabiliwa kwa shtaka moja la kuvunja nyumba mchana na kuiba Kinyume na Kifungu cha 294 (1) (a) na (b) cha Sheria ya Kanuni ya adhabu,(Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022).

Mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 19 Juni, 2025 maeneo ya Gombe Kusini iliyopo Kata ya Itezi ndani ya Wilaya na Mkoa wa Mbeya.

 Mshtakiwa alivunja nyumba ya Willy Hermina Olomi na kuiba magodoro mawili, king'amuzi cha DSTV, kitanda, kabati la viatu, kioo na sweta la mhanga. 

Siku ya tukio 19 Juni, 2025 majira ya saa nane mchana Neema  Mlochi jirani wa Willy Hermina Olomi alisikia vitu vinavunjwa kwenye nyumba ya jirani yake ilihali mmiliki wa myumba hiyo yupo safari ndipo aliamua kuchungulia kwenye ukuta wa nyumba hiyo na kuona dirisha la nyumba hiyo limekatwa na mlango wa nyuma umefunguliwa. Jirani huyo aliamua kutoa taarifa kwa Baba mzazi wa jirani yake ili alete funguo za nyumba hiyo kwani mmiliki alikuwa nje ya nchi kimasomo. Aidha jirani huyo alitoa taarifa kwa kituo cha Polisi ambao walifika kwenye eneo la tukio. 

Baada ya Baba mzazi wa mhanga kufika nyumbani kwa mhanga alifungua mlango akiongozana na askari pamoja na uongozi wa eneo hilo walifanya upekuzi kwenye nyumba hiyo na kufanikiwa kumkuta mshtakiwa amejificha kwenye moja ya vyumba vya nyumba ya mhanga akiwa amevaa sweta la mhanga. 

Pia katika upekuzi huo walibaini kuwa dirisha la grill lilikuwa limekatwa, vitasa saba vya milango vimevunjwa na baadhi ya vitu kama vile magodoro mawili na kitanda vilikuwa njee ya nyumba.
 
Aidha, baada ya mshtakiwa kukamatwa alipohojiwa alikiri kutenda kosa hilo mbele ya uongozi wa mtaa na wananchi mbalimbali.

Jumla ya mashahidi sita (6) wa upande wa Jamhuri walitoa ushahidi na mtuhumiwa alijitetea mwenyewe.

Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.