MAGEREZA YAPONGEZA TAASISI ZA HAKI JINAI KWA UTENDAJI MZURI
Mkuu wa gereza Kuu Ukonga, Kamishna Msaidizi wa Magereza Juma Mwaibako ametoa pongezi kwa taasisi zinazounda mnyororo wa haki jinai kwa utendaji mzuri ambao umeleta tija kubwa na kupunguza sana msongamano wa Mahabusu gerezani.
Aidha amepongeza pia ushirikiano wanautoa katika uendeshaji wa mashauri ya jinai kupitia kaguzi za UTATU zinazofanyika katika gereza hilo ambazo zimesaidia haki kupatikana kwa kesi nyingi kukamilishwa upelelezi na kusikilizwa mahakamani.
Kamishna Msaidizi wa Magereza amebainisha hayo wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Mashtaka akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Cyprian Chalamila na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Bw. Aretas Lyimo walipotembelea Gereza Kuu Ukonga tarehe 20 Novemba, 2024 ikiwa ni muendelezo wa ziara ya siku tatu ya kutembelea magereza katika Mkoa wa Dar es saalam.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Cyprian Chalamila amesema kuwa changamoto zote zilizowasilishwa zimepokelewa na zitafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo.
Akiongea na wafungwa wa gereza hilo amesema “Tunashukuru kusikia kwamba mmejifunza mengi mazuri mkiwa hapa na mkitoka mtaenda kuwa raia wema na tunawaahidi kuwa changamoto mlizoziwasilisha kwetu zitafanyiwa kazi na mtapata mrejesho ndani ya wiki mbili tangu leo.”
Aidha, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Bw. Aretas Lyimo, ameeleza kuwa, kupitia changamoto zilizopokelewa katika ziara hiyo imesaidia kupima utendaji kazi wao na utendaji wa wale waonaowasimamia ambapo amesema “Ziara hii imekuwa chachu kubwa kwetu ya kuboresha sehemu zenye changamoto ili kuhakikisha haki za mahabusu na wafungwa zinalindwa ipasavyo”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu wakati akihitimisha ziara ya kutembelea magereza ya mkoa wa Dar es saalam, ameipongeza timu nzima ya haki jinai Jijini Dar es salaam kwa kupunguza msongamano wa Mahabusu katika gereza la Ukonga ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Akizungumza na timu aliyoambatana nayo katika ziara hiyo DPP Mwakitalu amesema “Tukikamilisha upelelezi na uendeshaji wa kesi kwa wakati itasaidia kuwapunguzia mzigo wanaowatunza mahabusu na kuondoa msongamano gerezani, hivyo niwatie moyo wa kuendelea kuwahudumia wananchi kwa misingi ya haki.”