Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MASHIRIKIANO KATI YA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA NA UNODC YAZIDI KUIMARIKA KATIKA KUTOKOMEZA KESI ZA UKATILI WA KIJINSIA
04 Sep, 2025
MASHIRIKIANO KATI YA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA NA UNODC YAZIDI KUIMARIKA KATIKA KUTOKOMEZA KESI ZA UKATILI WA KIJINSIA

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amefungua mafunzo juu ya namna ya ushughulikiaji wa Makosa ya Ukatili wa Kijinsia kwa Mawakili wa Serikali ambao ni baadhi ya Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya na Waendesha Mashtaka Viongozi 50 yanayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 4 Septemba, 2025 katika Hotel ya Four Points by Sheraton Jijini Dar es salaam.

 Mafunzo hayo maalum kwa Waendesha Mashtaka yameandaliwa na Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu  (UNODC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kuwajengea uwezo washiriki hao katika kupambana na kesi za Ukatili wa kijnsia.

 Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Mashtaka  alitoa shukrani kwa UNODC kwa kufadhili na kusaidia kufanikisha mafunzo haya muhimu ambayo yanaakisi dhamira ya kujenga jamii yenye usawa kwa raia wote, hususani kwa  wanawake na watoto. 

 Pia alimshukuru  Bi. Linda Naidoo ambae ni Mratibu wa  UNODC kwenye masuala ya Ukatili wa Kjinsia kutoka ofisi za SADC pamoja na timu yake nzima kwa kuratibu mafunzo haya muhimu.

 “Kama Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tuna ufahamu mzuri kwamba mapambano dhidi ya Ukatili wa kijinsia yanahitaji jibu thabiti la haki linalomzingatia manusura. hii si tu kuhusu kuwafikisha wahalifu mahakamani bali pia kurejesha heshima, kulinda manusura, na kutuma ujumbe wazi kwamba Ukatili wa Kijinsia hauna nafasi katika jamii yetu.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.

Alieleza pia Ufanisi wa Mashtaka kuhusu mashauri ya unyanyasaji wa kijinsia unahitaji ushirikiano mzuri baina ya Waendesha Mashtaka, Polisi, Wafanyakazi wa Afya, Maafisa wa Ustawi wa Jamii, na Viongozi wa Kijamii. Tumekusudia kukuza njia ya ushirikiano ambapo taarifa zinashughulikiwa kwa ufanisi, wahanga wanapata msaada wa kina, na wahalifu wanawajibishwa kikamilifu.

Aidha, aliwahimiza washiriki hao kutumia fursa hii si tu kuboresha ujuzi bali pia kuimarisha dhamira haki, usawa, na utu.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka  Bi. Bibiana Kileo aliwaasa washiriki wa mafunzo haya kuwa wamepata nafsi adimu sana hivyo  waitumie   kuhakikisha wanapata uelewa ambao utaleta tija kwa taasisi na wadau wengine. Mwisho alimkaribisha Mkurugenzi wa mshtaka kuweza kufungua kikao.

Naye Mratibu wa  UNODC kwenye masuala ya Ukatili wa Kjinsia kutoka ofisi za SADC Bi. Linda Naidoo aliipongeza  Ofisi ya Taifa ya Taifa ya Mashtaka akiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu kwa juhudi wanazozitoa katika kupambana na kesi za Ukatili wa Kijinsia hususani kwa wanawake na watoto hivyo  amewataka kutokukata tamaa na zaidi kuendelea kukuza mashirikiano baina yao ili kuweza kutokomeza ukatili huo kwani unaleta  huzuni na kurudisha maendeleo ya kiuchumi katika jamii kwa ujumla.