MASHTAKA SPORTS CLUB YAONDOKA NA KOMBE PAMOJA NA MEDALI SHIMIWI

Katika hafla ya kuhitimisha Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyofanyika mkoani Morogoro, Mashtaka Sports Club imeibuka na ushindi wa kupata zawadi ya kombe moja na medali mbili kutoka katika mbio za baiskeli kilometa 50 na riadha mita 200.
Mashindano hayo ya SHIMIWI yamehitimishwa tarehe 5 Oktoba, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene.
Mshindi wa mbio za baiskeli kilometa 50 kutoka Mashtaka Sports Club iliwakilishwa na Bw. John Mgave ambaye aliibuka kuwa mshindi wa tatu na kukabidhiwa kombe moja na medali moja, na kwa upande wa riadha mita 200 iliwakilishwa na Judith Malata ambaye pia aliibuka na kuwa mshindi wa tatu na kukabidhiwa medali moja.
Katika hatua nyingine, Mashtaka Sports Club imepokea zawadi mbili za medali ambazo zimetolewa na Uongozi wa SHIMIWI ikiwa ni ishara ya kuutambua mchango wao katika kushiriki kwenye Mashindano hayo. Zawadi hizo zimekadhiwa kwa viongozi wa Mashtaka Sports Club ambao ni Mwenyekiti na Katibu wa Mashtaka Sports Club.
Akizungumza baada ya mashindano, Mwenyekiti wa Mashtaka Sports Club Bw. Juma Mahona amesema Kwa ujumla mashindano yameisha kwa mafanikio kwa kuwa timu ya kamba ya wanawake ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali huku timu ya kamba wanaume ikiishia hatua ya robo fainali. Na timu ya Mpira miguu ilitolewa katika hatua ya kumi na sita bora.
“Haya ni mafanikio Kwa Mashtaka Sports club Kwa kuwa ni mara ya pili kushiriki katika mashindano haya". Amebainisha hayo Mwenyekiti Mahona