MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA AINA YA BHANGI

Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Mbeya imemhukumu Hekima Adamu Mwakitalu kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kosa la kukutwa na Dawa za Kulevya aina ya bhangi.
Hukumu hiyo imesomwa tarehe 29 Agosti, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu Mhe. Andrew Scout baada ya kuridhika na ushahidi uliwasilishwa na upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo ya jinai Na. 20127 ya mwaka 2025, Bw. Mwakitalu mkazi wa Kijiji cha Muvwa - Mbeya alitenda makosa hayo mnamo tarehe 20 Novemba, 2024.
Imethibitika kwamba siku ya tukio aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Upelezi Wilaya ya Kipolisi Mbalizi alipata taarifa fiche kuwa mshtakiwa alikuwa akijihusisha na kilimo haramu cha bhangi katika shamba lake huko kijiji cha Muvwa.
Baada ya kupata taarifa hiyo na kuifuatilia, saa sita usiku askari polisi wakiongozwa na Mtendaji wa Kijiji cha Muvwa walifika nyumbani kwa mshtakiwa na baada ya utambulisho, Mshtakiwa aliwaongoza askari hadi katika shamba lake.
Ukaguzi wa shamba, ulifanyika na ndipo miche 23 ya bhangi ilipatikana ambayo tayari ilishakuwa imeng'olewa na kukusanywa katikati ya shamba.
Baada ya kuhojiwa mshtakiwa alikiri kuwa shamba ni lake na ile miche aling'oa kwa ajili ya kuiweka kwenye mfuko ili akauze.
Askari walimkamata mshtakiwa na kuhodhi miche hiyo 23.
Miche hiyo ilipelekwa katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi na ilithibitika kuwa ni miche ya bhangi yenye uzito wa Kilo 4.8.
Jumla ya mashahidi sita wa upande wa Jamhuri walitoa ushahidi na vielelezo vitano vilitolewa. Mtuhumiwa alijitetea mwenyewe.
Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mbeya