NAIBU WAZIRI MKUU, ATOA WITO WA KUPIMA AFYA KWA WASHIRIKI WA MICHEZO YA SHIMIWI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ametoa wito kwa watumishi wa umma nchini kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, hususan kabla ya kushiriki mashindano mbalimbali ya michezo, ikiwemo Mashindano ya SHIMIWI.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo leo tarehe 7 Septemba, 2025 wakati akifungua rasmi michezo ya 39 ya SHIMIWI yanayofanyika Jijini Mwanza.
Mashindano hayo yanahusisha timu kutoka Wizara, Mikoa na Taasisi mbalimbali za Serikali, yakiwa na lengo la kukuza mshikamano, kuboresha afya na kubadilishana uzoefu wa kikazi.
Katika hotuba yake, Dkt. Biteko ameeleza kuwa michezo si burudani pekee bali pia ni ajira na njia muhimu ya kuimarisha afya. Ameongeza kuwa sekta ya michezo imekua kwa kasi, ambapo mwaka wa fedha 2023/2024 imepanda kwa asilimia 18, huku mashindano ya SHIMIWI yakichangia ukuaji huo.
Amewataka washiriki kuonyesha nidhamu, heshima na upendo sambamba na kuwataka washiriki kuutumia muda wa mashindano hayo kujenga mahusiano chanya kazini na kuepuka uhasama, akisisitiza kuwa wote wanahudumia taifa na wananchi kwa pamoja.
Akitilia mkazo dhana ya kubadilishana uzoefu, Dkt. Biteko amesema mashindano hayo ni fursa ya kipekee kwa taasisi mbalimbali kubuni mbinu za kuongeza ufanisi na tija mahali pa kazi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko amewasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wa SHIMIWI na watumishi wote wanaoshiriki ambapo Rais, kupitia ujumbe huo, ameeleza matumaini yake ya kuona michezo hiyo inakua na kuleta tija zaidi katika afya na utendaji wa watumishi wa umma.
Naye Mwenyekiti wa Michezo kutoka Mashtaka Sports Club Bw. Juma Mahona ameeleza kuwa ofisi hiyo inashiriki kwa mara ya tatu, katika mashindano hayo ambayo yamekuwa na tija kwa watumishi wake kwa kuimarisha afya, mshikamano, na ufanisi kazini.
Baadhi ya wachezaji kutoka Mashtaka Sports Club akiwemo Godfrey Nugu na Judith Kyamba wamepongeza uongozi wao kwa kuwawezesha kushiriki mashindano hayo kwa kusema kuwa michezo imekuwa nyenzo muhimu ya kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha afya yao kwa ujumla.
Ufunguzi huo umefanyika katika viwanja vya CCM Kirumba, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu,Bw. Simon Ntobi pamoja na wachezaji na viongozi wa timu shiriki.