”Ni wakati sahihi sasa wa kutumia Intelijensia ili kuweza kutambua mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu.” Mkurugenzi Makondo

Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bi. Pendo Makondo amesema ni wakati sahihi sasa kwao wa kutumia Intelijensia ili kuweza kujua mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu, kwani wahalifu wengi wamekuwa wakitenda uhalifu pasipo kuguswa na mkono wa Sheria na wengine wengi kuharibu upelelezi na uendeshaji wa kesi katika hatua mbalimbali za kimashtaka ili wasiweze kupatikana na hatia.
“Kutokana na ukweli huu Ofisi yetu itaendelea kuandaa na kutoa mafunzo mbalimbali kama haya kwa Maafisa Viungo wa Waendesha Mashtaka wengi zaidi katika siku za usoni. Hii itasaidia kupata uelewa zaidi na kutambua zaidi mbinu zinazotumika kuharibu upelelezi na zinazozorotesha uendeshaji wa mashauri na hatua gani za kuchukua ili kunusuru kesi hizo.”
Mkurugenzi Msaidizi Makondo ameyasema hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza wakati akihitimisha Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma kuanzia tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.
Aidha, Mkurugenzi Msaidizi Makondo amefafanua kuwa mafunzo hayo yamewapatia fursa ya kujifunza na kujadiliana juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utendaji kazi ikiwemo kuangalia dhana nzima ya Udhibiti wa Upelelezi wa Mashtaka pamoja na mbinu za kutatua changamoto zinazojitokeza katika upelelezi na uendeshaji wa mashtaka na namna ya kuzikabili changamoto hizo, Ulinzi wa mashahidi na watoa taarifa wakati na baada ya upelelezi na uendeshaji wa kesi, Matumizi ya Intelijensia wakati wa upelelezi na uendeshaji wa mashtaka, Umuhimu wa uzalendo, weledi, uadilifu, utunzaji siri katika utendaji kazi wa kila siku, Hatua za kufuata katika Ushughulikiaji wa taarifa za kiintelijensia na namna ya kushughulikia wahanga wa makosa ya Ukatili wa Kijinsia wakati wa upelelezi na uendeshaji wa kesi.
Mkurugenzi Msaidizi Makondo amesema mafunzo waliyoyapata yamewawezesha kupata uelewa wa kutosha juu ya Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi pamoja na majukumu yao kama Maafisa Viungo wa idara hiyo.
“Ni matumaini yangu kuwa elimu na ujuzi mlioupata hapa sio tu mtaenda kuutumia katika maeneo yenu ya kazi lakini pia kuwashirikisha watumishi wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.’’ Amefafanua Mkurugenzi Makondo.
Sambamba na hilo Mkurugenzi huyo amewaasa maafisa hao kuwa elimu na ujuzi waliopata katika mafunzo hayo yakawasaidie katika kufanya uratibu makini katika upelelezi na uendeshaji wa kesi wenye tija ili kuhakikisha kila muhalifu anapata haki yake au adhabu anayostahili na sio kuachiwa mahakamani kutokana na sababu za kiufundi zinazotokana na upelelezi au uendeshaji wa kesi usiofuata masharti ya kisheria katika kuthibitisha kosa.
“Kupitia mafunzo haya nina imani mtatoka na kuwa mabalozi wazuri huko muendako, tunaamini mtakaa na Waendesha Mashataka wenzenu na mtawapa kile ambacho mmejifunza ndani ya siku tatu mlipokuwa mahali hapa na kuwasaidia katika kuboresha uendeshaji wetu wa mashtaka.” Amesema Mkurugenzi Msaidizi Makondo
Aidha, Mkurugenzi Msaidizi Makondo ametoa shukrani kwa niaba ya Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo kwa kuridhia mafunzo haya kufanyika kwa ukamilifu hadi kufikia hatua ya kuhitimishwa.
Pia alitoa shukrani kwa watoa mada kutoka Ofisi ya Usalama Serikalini, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kutoa elimu kwao licha ya majukumu…