OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAUNGANA NA MAMIA KATIKA MAZISHI YA MTUMISHI DAMAS KIYIZI
Mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kakonko, wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka baadhi ya mikoa, ndugu, jamaa na marafiki, wameungana katika mazishi ya Marehemu Damas Gerald Kiyizi aliyekuwa dereva Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Singida, mazishi yaliyofanyika tarehe 13 Oktoba, 2025 kijijini kwao Kiyizi, Kata ya Kakonko, Mkoani Kigoma.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo alieleza kuwa marehemu Damas Kiyizi alikuwa mtumishi wa mfano, mwenye maadili, mwaminifu, mchapakazi na mnyenyekevu, aliyeheshimu watu wote.
“Tumempoteza mtu muhimu sana, Marehemu alikuwa si tu mwajiriwa wa Serikali bali Mtumishi mwaminifu, mnyenyekevu, na mwenye moyo wa kujituma, aliyeipenda kazi yake na kufanya kwa bidii kila kazi aliyokabidhiwa,” alieleza Bi. Kileo.
Aliongeza kuwa katika kipindi chote alichohudumu, marehemu alionyesha moyo wa kujitolea, pamoja na mshikamano na wenzake.
Bi. Kileo aliihimiza familia ya marehemu kuendeleza mshikamano, upendo na umoja ili kuyaenzi maisha ya marehemu, na akawaasa wote walioguswa na msiba huo kuendelea kushikamana na familia ya marehemu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bw. Simon Ntobi, alitoa salamu za pole kwa familia na kueleza kuwa maisha ya mwanadamu hapa duniani ni ya muda mfupi, hivyo kila mmoja anatakiwa kuyaishi kwa hekima, nidhamu na uaminifu.
Katika hatua nyingine familia ya marehemu wameishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kufanya kazi na marehemu katika utumishi wake na kisha kushirikiana na familia tangu msiba ulipotokea na hatimaye mazishi.
Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Singida Bi. Mercy Ngowi, akisoma wasifu wa Marehemu alisema kuwa Damas Kiyizi alizaliwa tarehe 21 Januari 1975, katika familia ya watoto saba wa Mzee Gerald Kiyizi . Marehemu alikuwa mtoto wa mwisho katika familia hiyo.
Marehemu Damas Kiyizi ameacha pengo kubwa, lakini pia ameacha somo na mfano wa kuigwa katika utumishi wa umma — uadilifu, upendo, bidii na uaminifu.