"Rushwa isipodhibitiwa uchumi utayumba"- DPP

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema rushwa isipodhibitiwa kikamilifu itasababisha uchumi wa nchi kuyumba hali itakayochangia wananchi kutopata huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya, maji, barabara na maendeleo ya jamiii.
Mkurugenzi wa Mashtaka ameeleza hayo wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu ( Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kilichofanyika tarehe 8 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.
Kikao hicho cha Menejimenti kinalenga kufanya tathmini ya kazi na kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya taasisi hizo katika kufanya kazi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wote na wananchi wanapata huduma bora.
Mkurugenzi Mwakitalu ameitaka Menejimenti kufanya kazi kwa weledi, umakini na pia kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria.
"Kazi zetu zinagusa haki za watu, zinagusa maisha ya watu, maamuzi tunayoyafanya yote yanagusa haki za watu, tumeaminiwa na kupewa dhamana hii." Amefafanua hayo DPP
Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka amewasihi Menejimenti kushiriki kikamilifu kikao hicho kwani michango yao ya thamani inahitajika sana ili kuweza kutoka na maazimio ambayo yatasaidia kuboresha utendaji kazi wao kwa mwaka huu mpya.