Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

Tumieni Mwongozo wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashauri ya Makosa ya Kimtandao Ipasavyo." - Mhe. Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi
14 Feb, 2025
Tumieni Mwongozo wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashauri ya Makosa ya Kimtandao Ipasavyo." - Mhe.  Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi

Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa rai kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kote nchini kutumia ipasavyo Mwongozo wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashauri ya Makosa ya Kimtandao  uliozinduliwa  tarehe 13 Februari, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma. 

Alisema makosa ya mtandao yamekuwa yakiongezeka kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuleta athari za ukuaji wa uchumi na kuhatarisha utawala bora na haki za binadamu. 

Naibu Waziri Mahundi alizitaja miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ni Uandaaji wa miongozo mbalimbali juu ya matumizi bora ya mitandao, Uundwaji wa vitengo mbalimbali katika taasisi za Serikali mahususi kwa ajili ya kushughulikia makosa ya mtandao, Uanzishaji na urekebishaji wa sheria mbalimbali ili kudhibiti na kutoa adhabu dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao zikiwepo Sheria ya Makosa ya Mtandao (The Cyber Crimes Act, 2015), Sheria ya Miamala ya Kielektoniki (Electronic Transaction Act, 2015) na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektoniki na Posta (Electronic and Postal Communication Act, 2010) ikiwa ni pamoja na uundwaji wa kanuni mbalimbali.

Aidha, alisema Serikali imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na vyombo vya kutoa huduma vinavyotumia mtandao, ndani na nje ya nchi ili kupambana na makosa ya mitandao nchini.

Alisema lengo la mwongozo huu ni kuwawezesha Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wanaoshughulikia kesi za kimtandao kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kiwango kinachofanana. 

Matumizi sahihi ya Mwongozo huo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti tatizo la ushughulikiaji usio sawa wa mashauri ya Mtandao, hususan katika vipengele vya Upelelezi, Uandaaji wa Hati za Mashtaka, Uendeshaji wa mashauri Mahakamani pamoja na uandaaji wa Hati nyingine zinazowasilishwa Mahakamani kwa kuwa makosa hayo uhusisha mbinu za kisasa ambazo zinahitaji umakini mkubwa katika kupeleleza na kuendesha kesi mahakamani. 

Alihitimisha hotuba yake kwa kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kufanikisha maandalizi ya Mwongozo huu na kusema ni matumaini yake kuwa, Mwongozo huu utaleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa kazi na hatimaye kuisaidia Serikali kufikia malengo yake ya kitaifa katika kudhibiti vitendo vya Makosa ya Kimtandao.