WAAJIRIWA WAPYA WASISITIZWA KWENDA KUITEKELEZA MIKAKATI ILIYOWEKWA NA OFISI

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka Waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwenda kuitekeleza mikakati iliyowekwa na ofisi hiyo ikiwa ni pamoja na lengo la kuongeza ushindi wa kesi mahakamani.
Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati akihitimisha Mafunzo elekezi ya awali kwa Waajiriwa Wapya wa Ofisi yaTaifa ya Mashtaka (Orientation and Basic Induction Course) yaliyofanyika tarehe 01 hadi 04 Julai, 2025 Mkoani Iringa.
Mkurugenzi Mwakitalu amebainisha kuwa matarajio yao ni kutimiza lengo la kusimamia mashtaka ya jinai kwa ukamilifu, uadilifu na kuibuka na ushindi usiopungua asilimia 85.
“Kwa baadhi ya Mikoa na Wilaya tayari kwa asilimia kubwa wameweza kufikisha lengo tulilolianza la kufikisha asilimia 85 ya kushinda kesi mahakamani. Katika ziara zangu nimefurahi na kufarijika kukuta mahali pengine kesi imechukua wiki tatu toka iliposajiliwa hadi kufikia hukumu yake na matokeo yalikuwa ni mazuri.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.
Aidha Mkurugenzi Mwakitalu amesema ni imani yake kuwa kwa kipindi chote tangu walipoanza mafunzo hayo wamepata dozi ya kutosha ya kuwafanya kuwa tayari kutekeleza majukumu kwa kada zao katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hivyo amewaasa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu, upendo na kwa maarifa yao yote waliyonayo.
“Tunataka Ofisi hii iwe ni ofisi ya kwanza katika kusimamia haki, na haki ionekane imetendeka na ninyi ndio tunaowategemea.” Amefafanua Mkurugenzi wa Mashtaka.
Pia amewataka Makatibu Sheria kwenda kufanyia kazi kwa ukamilifu suala la takwimu na utunzaji kumbukumbu kwenye rejista na mfumo, kwani kuwepo kwa takwimu zilizo sahihi zinawasaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi na kwa wakati.
Aidha amewataka Madereva kuzingatia sheria na kanuni za barabarani ikiwa ni pamoja na kutunza vyombo vya usafiri walivyokabidhiwa na ofisi.
“Magari machache tuliyonayo haya mkayatunze vizuri, hatutamvumilia dereva yeyote ambae kwa uzembe atasababisha uharibifu wa Rasilimali tulizonazo na kuhatarisha maisha ya watumishi na wananchi wengine ambao wanatumia barabara za umma.’’ Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka Waajiriwa Wapya kwenda kuiheshimisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuibeba bendera ya Ofisi kwa kuwahudumia wananchi kwa upendo pamoja na wadau wao,lakini pia kwenda kuishi kwa mshikamano na umoja.
Aidha amewataka kuwa mstari wa mbele na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika majukumu yao ya kila siku.
Naye mmoja wa washiriki wa Mafunzo hayo ambae ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mtwara Bw. Thimotheus Sullusi akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine ameushukuru uongozi wa Ofisi hiyo mafunzo mazuri waliyoyapata na kuahidi kuyazingatia yale yote waliyofundishwa kwenda kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuweza kuiheshimisha Ofisi hiyo wakati wote.