Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

WAZIRI KABUDI AHIMIZA USHIRIKIANO KWA TAASISI ZINAZOSIMAMIA HAKI JINAI
10 Oct, 2024
WAZIRI KABUDI AHIMIZA USHIRIKIANO KWA TAASISI ZINAZOSIMAMIA HAKI JINAI

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amezitaka Taasisi zinazounda haki jinai kujenga utamaduni wa kuwa pamoja, kufanya kazi pamoja, kusaidiana  na kuwezeshana ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Kabudi amebainisha hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa kinachofanyika tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.

Prof. Kabudi amesema kuwa Taasisi zinazosimamia Haki Jinai nchini zinatakiwa kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata Haki zao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia misingi ya haki ili kuhakikisha amani, utulivu na umoja vinatamalaki kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema umoja huo wa Utatu uliundwa kwa lengo la kurahisisha utendaji wao wa kazi na pia kutatua changamoto wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ambazo kwa namna moja ama nyingine zinachelewesha ama kukwamisha haki za watu.

"Tuliamua kila mwaka tuwe tunakutana Menejimenti ya Utatu na Viongozi wa ngazi za mikoa ili kujadiliana na kutathmini yale ambayo tumeyafanya pamoja na kuweka mikakati ya mwaka mwingine unaokuja, na tumekuwa na mijadala mizuri, mawasiliano na mada mbalimbali na kuongeza ufanisi katika majukumu yetu". Amefafanua hayo Mkurugenzi DPP

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna Ramadhani Kingai amesema ushirikiano wao umeleta manufaa makubwa kwao katika utekelezaji wa utoaji haki  katika jukwaa la haki jinai. 

"Ni rai yangu kuendeleza na kuimarisha ushirikiano huu hususani katika kushughulikia makosa yanayovuka mipaka hivyo ni muhimu kukuza ushirikiano huu sio tu kwa Taasisi zetu bali kuwa na mashirikiano kutoka katika taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi." Amebainisha hayo DCI Kingai.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Bw. Crispin Chalamila ameeleza kuwa kupitia mashirikiano waliyonayo ya Utatu, ameshuhudia ongezeko la idadi za kesi zilizofunguliwa mahakamani baada ya kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka, aidha wamekuwa na vikao vya viongozi na watendaji katika ngazi za mikoa vinavyofanyika mara kwa mara na hivyo kusaidia kuharakisha maamuzi mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amebainisha kuwa kupitia mashirikiano hayo Waendesha Mashtaka watatu wa TAKUKURU wamepata vibali vya kuendesha kesi katika Mahakama Kuu na pia kuahidiwa vibali hivyo kuongezwa. Pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya kesi zinazofunguliwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutokana na vikao vya pamoja vya kupitia majalada.

"Ni matarajio yetu kwamba kupitia kikao hiki tutaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano huu ambao 
kimsingi unasaidia kuondoa malalamiko ya ucheweleweshwaji wa haki jinai" Amefafanua hayo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Bw. Mgeni Jailan Jecha ametoa pongezi na shukrani kwa Menejimenti ya Bara kwa mwaliko wa ushiriki katika kikao hicho cha Utatu kwani kutasaidia  kuimairisha zaidi mashirikiano ya sekta za Jinai baina ya Bara na Zanzibar, pia kujifunza na kupata uzoefu wa utendaji kazi kupitia kikao hicho cha Utatu.