WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AZINDUA MIONGOZO MIWILI KUTOKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefanya uzinduzi wa Miongozo ya Ushughulikiaji wa Kesi za Wanyamapori na Misitu pamoja na Kesi za Uvuvi Haramu kwa Waendesha Mashtaka na Wapelelezi.
Amezindua miongozo hiyo Jijini Arusha tarehe 19 Februari, 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa miongozo hiyo katika mkutano wa mafunzo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka nchini.
Dkt.Chana amesema miongozo hiyo itawasaidia wadau wa kesi hizo kuziendesha kwa haki na kuleta manufaa kwa rasilimali nchini.
"Jukumu la kulinda rasilimali zetu ni letu sisi wenyewe hivyo naamini wapelelezi na waendesha mashtaka kwa sasa mtasaidia kukomesha ujangili wa wanyamapori wetu, uvuvi haramu kwenye maziwa na bahari, lakini pia kukomesha uharibifu wa misitu yetu." Amezungumza hayo Mhe. Waziri
Aidha alisema rasilimali zilizopo nchini zinachangia pato la Taifa na fedha hizo zinafanikisha kuendesha shughuli mbalimbali za maendelo.
Amesema baada ya uzinduzi huo anawatahadharisha wanaojihusisha na ujangili wa rasilimali za Taifa kuacha kwani wadau wa maeneo hayo wamejipanga vizuri kuhakikisha wana komesha tabia hizo.
Dkt. Chana amesema Taifa haliwezi kuacha baadhi ya watu wakiendelea kuvuna rasilimali za nchi kwa manufaa yao peke yao, bila kufuata sheria ni lazima wadhibitiwe.
Awali akimakaribisha mgeni rasmi Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chama, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu alisema uzinduzi wa miongozo hiyo ina manufaa makubwa kwa maliasili nchini.
"Tumeona tuhuhishe muongozo wa Ushughulikiaji wa Kesi za Wanyamapori na Misitu na Muongozo wa Kesi za Uvuvi haramu sababu tumeona tusipokua makini katika kulinda rasilimali zetu kama bahari na maziwa yatabaki tupu kutokana na uvunaji haramu wa mazao haya unavyozidi kushamiri." Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu.
Alisema kuna wakati makosa hayo yanafanywa kwa kupanga kitaifa na kimataifa, hivyo kupitia miongozo hiyo itawasaidia kudhibidi uhalifu huo ndani na nje ya nchi.
Pia katika ukusanyaji wa ushahidi wa makosa hayo kupitia miongozo hiyo itasaidia kufanywa kisanyansi, teknolojia na kielekroniki na mafunzo hayo yatatolewa kwa wadau wa sekta hiyo nchi nzima kwa Waendesha Mashtaka kutoka Taasisi za utalii kama TANAPA, TAWA, NCAA, TFS, POLISI na TAKUKURU
Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mashataka nchini Bi. Javelin Rugaihuruza alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeona kuna umuhimu wa kuandaa mafunzo hayo ili kufundisha wadau mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu wa rasilimali nchini kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake Katto Wambua kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu(UNODC) ambao ndiyo wameandaa miongozo hiyo na kuwezesha mafunzo kwa Waendesha Mashtaka na Wapelelzi nchini alisema watatengeneza APP itakayowezesha kuisoma miongozo hiyo kwenye simu, pamoja na kusoma miongozo ya nchi zingine.