DPP AHIMIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Sylvester Mwakitalu amewaasa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa Umma ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Bw. Mwakitalu amebainisha hayo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka unaofanyika Oktoba 31 na 01 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Kwatunza Beach uliopo Ilemela Jijini Mwanza ambapo amesema kuwa licha ya wafanyakazi kudai maslahi na stahiki zao ni vema wakatimiza wajibu wao kwa wakati na kwa ufanisi.
“Nasisitiza uwajibikaji katika kazi zenu na katika kikao hiki msiwaangushe wenzenu waliobaki kwenye vituo vyenu vya kazi, kwa kuhakikisha mnatoa mapendekezo, maoni na kueleza changamoto zao ili kuwezesha kikao hiki kutoka na maazimio ya pamoja yatakoyowezesha kuweka mazingira bora ya utendaji kazi wetu na masuala yote yanayohusu utumishi”. amesema Bw. Mwakitalu
Mkurugenzi wa Mashtaka.
Aidha, Mwakitalu amesema uwepo wa Baraza la Wafanyakazi katika taasisi ni moja ya njia bora ya kupokea, kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kazi kutokana na jiografia ya nchi na hivyo kupitia wawakilishi wao kwenye baraza inalenga kuleta mitazamo chanya na kuboresha maisha ya watumishi.
Katika hatua nyingine Bw. Mwakitalu ameitumia nafasi hiyo kumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Bibiana Kileo ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye kimuundo wa baraza anaingia moja kwa moja kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema tangu kuasisiwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mwaka 2018 Ofisi imekuwa ikijadili na kupitia masuala mbalimbali yanayaohusu wafanyakazi ili kutathmini na kuona ni kwa namna gani Ofisi imeweza kutekeleza maazimio ya mabaraza yaliyopita.
Bibiana amesema Baraza la Wafanyakazi husaidia kuwapa nafasi ya kutafakari masuala mbalimbali yanayowahusu zikiwepo changamoto zao ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na umahiri walionao sambamba na kuwapongeza watumishi wote kwa kufanya kazi kwa moyo wa uaminifu ili kusaidia jamii kupata haki zake.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi amesema baraza hilo la tatu la wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka lina jukumu kubwa la kuishauri taasisi ili maslahi ya wafanyakazi yaweze kupatikana kwa wakati.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Bw. Rugemalira Rutatina ameipongeza Ofisi ya Mashtaka kwa kulipa hadhi Baraza la Wafanyakazi kwa kuhakikisha wanapokea na kupitia changamoto za wafanyakazi katika mazingira rafiki na kuwapa nafasi ya kueleza changamoto zao ili tija na ufanisi wa kazi uweze kuonekana.
Rugemalira amewasisitiza wakuu wa Idara na Divisheni kuwahamasisiha wafanyakazi walio chini ya idara zao kujiunga na mabaraza ya wafanyakazi ili waweze kutoa maamuzi ya pamoja na si kungoja kuamriwa na kundi la wachache ambao ni wanachama hai wa baraza.
Kwa upande wake Afisa Kazi Mkuu Kanda ya Kati, Bw. Goodluck Luginga akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Kazi katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka amesema ni jukumu la watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa tija ili kuleta matokeo chanya kwa ajili ya umma.