Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

RAIA 7 WA IRAN WAFIKISHWA MAHAKAMANI LINDI KWA KUSAFIRISHA HEROIN KILO 504.36
04 May, 2021
RAIA 7 WA IRAN WAFIKISHWA MAHAKAMANI LINDI KWA KUSAFIRISHA HEROIN KILO 504.36

RAIA saba wa Iran akiwemo nahodha wa boti, Jan Miran (42) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha heroin zenye uzito wa kilo 504.36 na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 355.

Mbali na Miran, washtakiwa wengine ni Issa Ahmad(30), Amir Kasom (35), Salim Fedhmulhammad (20), Ikbal Mohammad(22), Mustaphar Bakshi (20) na Jawid Mohammadi(19).

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao Aprili 30, 2021 na jopo la mawakili wa Serikali waandamizi, Joseph Maugo na Juma Maige mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Maria Bantulayne.

Wakili Maige amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2021.

Kabla ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Bantulayne amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi

Akiwasomea mashtaka yao, Wakili Maugo amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa April 23, 2021 katika bahari ya Hindi eneo la Lindi wanadaiwa kusafirisha heroin yenye uzito wa kilo 504.36

Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine yenye uzito wa kilo 355.0.

Hata hivyo washtakiwa hao walitafutiwa mkalimani anayejua Kiirani kutokana na wao kutokujua lugha nyingine.

Hakimu Bantulayne baada ya kusikiliza shauri hilo, aliahirisha kesi hadi Mei 14, 2021 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.