Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

JELA MIAKA 30 KWA KOSA LA KUSAFIRISHA BANGI
27 Jul, 2026
JELA MIAKA 30 KWA KOSA LA KUSAFIRISHA BANGI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Rungwe imemhukumu  James Boyd Mwakalebela (26), kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la kusafirisha Dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 23.8.

Hukumu hiyo imesomwa tarehe 24 Julai, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya ya Rungwe, Mhe. Jackson Thomas Banobi baada ya Mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri.

Imeelezwa mahakamani hapo, katika kesi hiyo ya jinai Na. 5568/2026 Bw. James Mwakalebele  alikamatwa tarehe 07 Februari, 2026 majira ya saa 2:00 usiku katika Kizuizi cha Polisi Kayuki kilichopo Wilaya ya Rungwe kwenye Barabara Kuu ya Kyela Jijini Mbeya. 

Wakati wa ukamataji huo, mshtakiwa alikuwa ni abiria katika gari la abiria aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T.138 EAQ, akiwa na mizigo ya magunia mawili yaliyokuwa na majani makavu na mbegu za bangi zenye uzito wa kilogramu 23.8 yaliyohifadhiwa katika buti la gari hilo. 

Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani mnamo tarehe 13 Machi, 2026 ambapo alisomewa shtaka linalomkabili na kulikana. Katika usikilizaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi saba na vielelezo vitano vilivyoweza kuifikisha Mahakama kufikia uamuzi wa kumtia hatiani. 

Kesi hiyo iliendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.